PATA HABARI KWA WAKATI

Thursday 24 May 2018

AMEKATWA – ISHU NI MESSI, ICARDI KUTEMWA


 

LICHA ya kupachika mabao 29 katika msimu wa Serie A uliomalizika hivi karibuni, straika Mauro Icardi hatakuwamo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Argentina kitakachokwenda Urusi kushiriki fainali za Kombe la Dunia.

Kuachwa kwake katika kikosi cha mastaa 23 watakaokuwa na timu ya taifa ya nchi hiyo, kumewaacha hoi mashabiki wengi wa kandanda.

Inawezekana vipi Icardi, ambaye amegawana tuzo ya mfungaji bora wa Serie A na Ciro Immobile wa Lazio aishie kuzifuatilia fainali hizo kupitia televisheni yake ya nyumbani?

Lakini je, mbona takwimu za msimu uliokwisha zinaonesha kuwa Icardi amewazidi kwa idadi ya mabao mastaa Paulo Dybala (22) na Gonzalo Higuain (16) walioitwa kikosini?

Akiuzungumzia uamuzi wake wa kumpotezea, kocha Sampaoli alisema amechagua wachezaji wanaoendana na aina ya uchezaji wa Argentina.

“Icardi, Perotti, Papu Gomez na Lautaro Martinez hawatakuwa na sisi Urusi, lakini ni wachezaji wazuri, wanaoweza kuwa katika eneo letu la ushambuliaji,” alisema Sampaoli.

Mpachikaji mabao wa zamani wa kikosi hicho, Hernan Crespo, amekosoa kitendo hicho cha Icardi kuachwa katika msafara utakaoelekea Urusi.

Crespo alisema Messi ana ushawishi mkubwa katika uteuzi wa kikosi cha Argentina, lakini bahati mbaya aliyonayo Icardi ni kutokuwa rafiki yake.

“Ninavyoona, ni kwa sababu si rafiki wa Messi, sijui kama nimekosea… Nafikiri (kuachwa) ni kosa kubwa. Argentina inamhitaji sana straika kama yeye,” alisema.

Ikumbukwe kuwa, Icardi amekuwa katika wakati mgumu wa kuitwa kikosini tangu ilipobainika kutoka kimapenzi na mke wa mchezaji mwenzake, Maxi Lopez, wakati nyota hao wakiichezea Sampdoria.

Inafahamika wazi kuwa Lopez ni rafiki mkubwa wa nahodha wa timu hiyo, yaani Messi, hivyo, kitendo hicho cha Icardi ‘kuchepuka’ na bibiye Wanda kilimkera pia mchezaji huyo wa Barcelona.

Lakini, tuhuma hizo za kuzuia Icardi kuitwa kikosini ziliwahi kukanushwa vikali na Messi mwenyewe, aliyesema hana mamlaka hayo ya kupendekeza anayetakiwa kucheza Argentina.

Ukiacha Messi, tukio lake hilo lilimfanya Icardi kuchukiwa nchini humo na hadi leo hii, mkongwe Diego Maradona amekuwa akimponda.

Katika moja ya mechi zake za hisani, Maradona aliulizwa juu ya uwezekano wa straika huyo kwenda katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014.

“Huwa siwazungumzii wasaliti,” alisema Maradona na kuongeza kuwa, kama angekuwa kocha wa Argentina, basi nyota huyo angekuwa chaguo la saba katika orodha ya mastraika wake.

“Kabla ya kumuita Icardi, ningeanza na (Daniel) Bazan Vera (mshambuliaji aliyekuwa na umri wa miaka 43 kipindi hicho. Ningependa aachwe tu.”

Hata hivyo, wakati Maradona anayasema hayo, tayari Icardi alikuwa ameshazipasia nyavu mara 14 akiwa na Inter na Argentina ilikuwa chini ya kocha Edgardo Bauza.

No comments:

Post a Comment